Utata mkubwa umeibuka kuhusu waraka halisi wa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’ uliosababisha Zitto Kabwe kuvuliwa wadhifa wake wa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema na kikao cha Kamati Kuu ya chama hicho kilichofanyika Novemba 20 - 22, mwaka huu.
Baada ya juzi, Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa Chadema, John Mnyika kuwaeleza wanahabari kuwa waraka uliochapishwa katika magazeti na mitandao ya kijamii, siyo halisi, aliyekuwa Mwenyekiti wa chama hicho Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba amejitokeza na kuutetea huku akidai kwamba huo unaodaiwa na uongozi kuwa ndiyo halisi umeghushiwa.
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), alivuliwa uongozi pamoja na aliyekuwa Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na Mwigamba kutokana na madai ya kuandaa waraka huo ambao Chadema kimesema ulikuwa unaeleza mbinu za uasi za viongozi hao ambazo zingetumika wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho jambo ambalo ni kinyume na katiba, sheria na itifaki zake.
Katika tamko alilotoa jana, Mwigamba alidai kwamba
kuna njama zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa Chadema ili kuubadili waraka halisi wa ‘Mkakati wa Mabadiliko 2013’ kwa lengo la kupoteza maana yake, huku akisisitiza kuwa waraka halisi hauna tatizo lolote.
Katika madai yake, Mnyika alisema waraka huo unaosambazwa na kuchapishwa, si ule uliowasilishwa na kujadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu na kuahidi kuutoa waraka halisi ambao una mambo makubwa na mengi zaidi.
“Waraka utakaotumika katika mashtaka yao siyo huo. Sisi tutautumia ule ambao uliwasilishwa katika Kamati Kuu ambao una mambo makubwa na mengi zaidi kuliko huo unaochapishwa sehemu mbalimbali, ikibidi tutautoa huo waraka halisi,” alisema.
Hata hivyo, jana Mwigamba alisema waraka halisi ni ule ambao upo katika kompyuta mpakato (Laptop) aliyonyang’anywa na wanachama wa Chadema, Oktoba 25, mwaka huu, katika mkutano mjini Arusha.
“Waraka uliosambazwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari na mitandao ya kijamii ni sahihi neno kwa neno kama nilivyousoma katika magazeti ya jana (juzi), pamoja na nakala iliyopo katika mtandao wa kijamii wa Jamii Forums.”
Aliongeza: “Ili kuthibitisha kwamba waraka ule ndiyo wenyewe, nawatumieni ‘soft copy’ kutoka kwenye kompyuta yangu kwani waraka huo uliibwa kutoka katika kompyuta hiyo ambayo nilirudishiwa baada ya wao kuikagua na kukuta waraka huo halisi.”
Mwigamba alisema waraka wake unatofautiana kwa kiasi kikubwa na ule ambao Chadema kinasema kuwa ndiyo halisi: “Lissu na wenzake wana mpango wa kuuchakachua waraka huu, lakini wamekwama.”
Alisema kuandaa waraka huo siyo uhaini kama ambavyo imekuwa ikielezwa na viongozi wa Chadema na kusisitiza kuwa ni waraka wa kusaka ushindi katika uchaguzi halali ndani ya chama hicho uliopangwa kufanyika Desemba mwaka huu na baadaye kusogezwa hadi Juni mwakani.
<<<Habari na mwananchi gazeti>>>