Interviews

Msanii, Nassib Abdul a.k.a Diamond ambaye tangu kuanza kwa mwaka huu amekuwa akiwika ndani na nje ya nchi, anazungumza kiundani na gazeti la Mwananchi amefanikiwa kiasi gani. Na hivi ndivyo mazungumzo yalivyokwenda:


Starehe:Hongera sana kwa kuugawa mwaka salama.

Diamond:Nashukuru sana kwani siku hizi kifo kipo mkononi.

Starehe:Tukiwa tunaugawa mwaka na wewe ni miongoni mwa wasanii waliofanya vizuri mwaka huu labda siri ya mafanikio yako ni nini?

Diamond:Kiukweli siri ya mafanikio yangu ni kujituma kwa bidii lakini zaidi ni malengo ambayo hujiwekea kabla ya mwaka kuisha kwamba mwakani nitafanya hivi na hivi.

Starehe: Kwa maana hiyo unataka kusema mafanikio yako uliyatarajia?

Diamond:Kulingana na mipango  yangu na malengo niliyojiwekea mwaka jana ni kama nilikuwa nawaza kupata mafanikio ingawa kwa kiasi kikubwa nilitegema zaidi mashabiki watakavyonipokea bila kusahau nini nitawapa.

Starehe:Enhee....

Diamond:Hiyo ndio siri pekee pamoja na kutegemea mashabiki lakini pia nilisoma soko la muziki linataka nini si unajua sasa hivi Dunia ni kama kijiji,kinachoimbwa Marekani kinakuja huku kwetu kama upepo lakini kuna nchi jirani ambazo kwa kiasi fulani tabia zetu zinafanana, hivyo hata ujumbe uliopo kwenye tungo zetu unaendana japo sio sana.Kabla ya kutoa wimbo ili mashabiki waupende inabidi uangalie mambo kama hayo.

Starehe:Unaonaje ushindani wa muziki kwa majirani zetu, yaani Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda n.k

Diamond:Kwanza kabisa nakuhakikishia kwa nchi za Afrika Mashariki Tanzania tupo vizuri kimuziki na ndio maana tunakubalika nchi zote tano,nasema hivyo kwa kuwa wanamuziki ambao tunafanya vizuri hapa nyumbani tupo wengi tofauti na nchi nyingine kati ya hizo tano ambazo labda msanii anayetamba ni mmoja mmoja.

Starehe:Mbona umejibu kwa kujiamini unaweza kunipa mfano hata mmoja kuthibitisha hilo?

Diamond:....Kicheko...mifano ipo mingi lakini mmojawapo ni kwamba hawezi kuja msanii kutoka kati ya nchi hizo akapata mashabiki wengi kutoka kwetu bila kushirikiana na wanamuziki wa hapa nyumbani, hiyo inaonyesha kuwa hawana uwezo kushinda sisi na ndio maana waandaji wamelitambua hilo na kuhakikisha akija mwanamuziki na wenyewe tunakuwepo ili kuwapa raha mashabiki wetu. Sisi tuna uwezo wa kwenda nchi nyingine na kupiga shoo bila kumshirikisha msanii kutoka nchi tuliyoenda.

Starehe:Hongera sana kwa niaba ya wanamuziki wenzako,lakini turudi kwako wewe binafsi ni shoo gani kali umepiga tangu kuanza kwa mwaka huu hadi kufikia sasa?

Diamond:Tabasamu pana....Kiukweli zipo mbili na nikitaja moja nitawapunja mashabiki wangu ambao kwa nia moja ama nyingine wananiunga mkono kila ninapofanya shoo.


Starehe:Mmh...ni zipi hizo Diamond?

Diamond:Nashukuru kwa kupata nafasi hii kwanza kabisa nawashukuru mashabiki wangu kwa jinsi walivyoniunga mkono katika shoo hizo,ambazo ni ile niliyopiga Mlimani

City ambayo niliipa jina la Diamond Are Forever,na ile niliyopiga Mbagala katika Ukumbi wa Dar Live kiukweli sitazisahau na ninasema ahsante sana mashabiki wangu.

Starehe:Bado hujatueleza vizuri kwa nini huwezi kuzisahau na unajivunia kuwa mwanamuziki kwa shoo hizo tangu mwaka huu uanze ?

Diamond:Huwezi amini kwenye shoo ya Mlimani City nilikusanya zaidi ya sh80mil za Tanzania na ya Mbagala nililipwa sh10mil bila utata wala longolongo yoyote.

Starehe:Zaidi ya kukusanya fedha nyingi nini kilikufurahisha na kujivunia.

Diamond:Sikufichi ni shoo ya Mbagala,kwa sababu ni shoo iliyokutanisha watu wa rika zote wakubwa, watoto,vijana na watu wa makamu walionifurahisha zaidi ni watoto kwa kuwa waliweza kunisubiri na hii ni faraja kwangu kwa kuwa nimeona ni kwa jinsi gani ninapendwa na kutoa burudani kwa watu wa rika zote nimefurahishwa sana na hilo.

Starehe:Kutokana na kiwango chako kupanda na hivi majuzi umepaform kwenye jumba la Big Brother ni wasanii Wangapi wa nje ambao wametaka kufanya kolabo na wewe.

Diamond:Hata kabla ya kwenda Big Brother ambayo na hiyo ni moja ya mafanikio kwangu,wasanii wengi wa nje ingawa sipendi kuwataja walikuwa wananiomba nifanye nao kolabo lakini kuna mambo yalinifanya niwe bize kidogo nikikaa vizuri kila kitu kitakuwa poa.

Starehe:Pamoja na mafanikio uliyoyapata wewe binafsi lakini hali ya muziki unaionaje.

Diamond:Nikitoa kulinganisha na nchi nyingine kama nilivyokujibu mwanzo, muziki unakuwa huku changamoto ikiwa kubwa kwa wanamuziki wakongwe kwa kuwa kuna wanamuziki wanaibuka, ingawa hawadumu kwenye fani lakini akitoa nyimbo inakuwa juu sasa kama hujasimama imara lazima uyumbe.

Starehe:Ndio unataka kusemaje hasa kwa hao wanaoingia na kutoka na kwa nyinyi wakongwe.

Diamond:Wanaoingia na kutoka sina komenti kwa kuwa labda hawakujipanga, kazi inabaki kwa wakongwe kuhakikisha wanapambana na changamoto hii,kwani kutolewa nishai na mwanamuziki chipukizi ni aibu.

Starehe:Mashabiki wako wategemee nini mwezi huu ambapo tupo katikati ya mwaka 2012.

Diamond:Kwanza kabisa kabla ya yote wakae mkao wa kula kupokea video ya wimbo wa 'Lala salama' na nimpende nani,nasema ni kali narudia tena ni kali wakae mkao wa kuburudika roho ,mwili,akili na macho pia kwa kuona kitu kizuri.