Monday, September 22, 2014

CHADEMA WASHIKIRIA MSIMAMO WAO

Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kimesisitiza
kufanya maandamano kuanzia leo hadi
Ijumaa wiki hii licha ya Polisi kuyapiga
marufuku.
Chama hicho kimesema maandamano
hayo yataenda sambamba na migomo na
mikutano ya hadhara na pia
yatawahusisha wananchi wa kawaida,
taasisi na wafuasi wa vyama
vinavyounda Umoja wa Katiba ya
Wananchi(Ukawa) ambavyo ni CUF,
NCCR-Mageuzi, NLD na DP.
Juzi na jana katika baadhi ya mikoa
wafuasi wa chama hicho walifanya
maandamano na kudhibitiwa na polisi.
Msemaji wa Jeshi la Polisi, Advera Senso
amewaonya wananchi kutoshiriki
maandamano hayo kwa maelezo kuwa
Bunge la Katiba linaendeshwa kwa
mujibu wa sheria, hivyo kufanya
maandamano kutaka lisitishwe ni sawa
na kuvunja sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari
jana katika ofisi za makao makuu ya
Chadema, Kigaila alisema maandamano
hayo yatafanyika asubuhi katika mikoa
mbalimbali nchini, Dar es Salaam
yatafanyika Jumatano.
Alisisitiza kuwa sababu zilizotolewa na
Polisi kusitisha maandamano hayo ni
kinyume na sheria ya Mabadiliko ya
Katiba, Katiba ya nchi, Sheria ya Vyama
vya Siasa na Sheria ya Jeshi la Polisi.
Alisema kitendo cha Polisi kuwakataza
kufanya maandamano ni kinyume na
Ibara ya 20 ya Katiba ya sasa, kifungu
cha 11 (1) cha sheria ya vyama vya siasa
ya mwaka 1992 na kifungu cha 43 hadi
45 cha sheria ya Jeshi la Polisi.
Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim
Lipumba ameunga mkono maandamano
hayo ya Chadema na kusema kuwa
chama chake kimejikita zaidi katika
kufanya mikutano ya hadhara kulaani
kuendelea kwa vikao hivyo vya Bunge.
Akizungumza jana, Profesa Lipumba
alisema CUF inaunga mkono kwa sababu
maandamano na mikutano ya hadhara
vinaruhusiwa kwa sheria namba tano ya
vyama vya Siasa ya mwaka 1992.
Alisema vyama vya siasa havitakiwi
kuomba vibali vya kufanya
maandamano na mikutano ya hadhara
kutoka kwa Polisi bali wanatakiwa kutoa
taarifa tu.
“Tunashangaa Jeshi la Polisi kujipa
madaraka ya kutoa vibali vya kufanya
maandamano na mikutano wakati
hakuna sheria inayowaruhusu kufanya
hivyo,” alisema Profesa Lipumba.

0 comments: