Siyo tetesi tena. Sasa ni rasmi
kwamba Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambaye
amekuwa akitajwa kuwania urais
amethibitisha wazi kuwa atagombea kiti
hicho katika uchaguzi mkuu mwakani.
Alitoa uthibitisho huo juzi akiwa London,
Uingereza ambako yuko katika shughuli za
kikazi. Hatua hiyo inaondoa uvumi ambao
umekuwapo kwa takriban miezi mitatu sasa
kwamba naye tayari ameingia katika
kinyang’anyiro hicho.
Pinda aliweka wazi nia ya kuelekea Ikulu
akisisitiza kuwa hajatangaza rasmi lakini
akasema kuwa ameanza harakati hizo
‘kimyakimya’. Alikuwa akijibu moja ya
maswali aliyoulizwa katika Kipindi cha Dira
ya Dunia kinachorushwa na Shirika la
Utangazaji la Uingereza (BBC).
Alitamka rasmi kuwania nafasi hiyo baada ya
kuulizwa kuwa anafikiri ni kiongozi gani
anayefaa kurithi mikoba itakayoachwa na
Rais Jakaya Kikwete.
“Mikoba ya Rais Kikwete inaweza
kuchukuliwa na yeyote atakayeonekana
mwisho wa safari kwa utaratibu wa chama na
ndani ya Serikali .... kama anafaa.
Waliojitokeza sasa ni wengi na mimi
ninadhani ni vizuri,” alisema Pinda.
Alipoulizwa kama yupo miongoni mwa wengi
alisema, “… umesikia kama nimo … basi
tukubali hilo na yeye Waziri Mkuu yumo. Hao
wote waliojitokeza pamoja na Waziri Mkuu
aliyejitokeza ni katika jitihada za kusema
hebu Watanzania nitazameni je, mnaona
nafaa au hapana?”
Thursday, October 23, 2014
7:04 AM
No comments
0 comments:
Post a Comment